Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

Wizara ya Ujenzi na JWTZ zaahidi kukuza ushirikiano


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, ameliomba Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara yake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara hiyo nchini.

Akizungumza katika kikao cha kufahamiana na kubadilishana uzoefu na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
Luteni Jenerali  Methew Edward Mkingile, Dkt. Chamuriho, amesema kuwa licha ya Wizara kutumia wataalam mbalimbali katika miradi ya Ujenzi, bado inahitaji ushirikiano na  wataalam kutoka katika Jeshi hilo.

“Nakupongeza kwa uteuzi uliopata, naamini kuwa uteuzi huu utakuwa chachu ya kuendeleza ushirikiano tuliokuwa nao na kusaidia katika mwendelezo wa utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na Wizara”, amesema Waziri Dkt. Chamuriho.

Aidha, Dkt. Chamuriho amesisitiza kuwa kutumia wataalam shirikishi kutoka katika Jeshi hilo imekuwa ni msaada mkubwa katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile, ameipongeza Wizara hiyo kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi hilo na kuwaamini katika kutekeleza miradi ya Wizara.

“Sisi tupo tayari na bado tutaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara na Taasisi za Serikali kama Sheria inavyotutaka, lengo ni kuhakikisha malengo na maendeleo ya nchi yanafikiwa”, amesisitiza Luteni Jenerali Mkingile.

Uongozi wa Wizara umekutana na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Methew Edward Mkingile, ikiwa ni siku kadhaa mara baada ya uteuzi wake ambapo pamoja na mambo mengine ziara hii ilikuwa na lengo la kuendeleza na kukuza ushirikiano baina ya Taasisi hizo.