Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

WAZIRI MBARAWA AWATAKA MAKANDARASI KUCHANGAMKIA FURSA


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameitaka Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), kutumia fursa  zinazotolewa na Serikali kwa wakandarasi wazawa kujenga miradi kwa viwango bora na kuikamilisha kwa wakati.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashauriano wenye kauli mbiu “Umuhimu wa Mchango wa Makandarasi Katika Uchumi wa Tanzania” Prof. Mbarawa amesema Serikali inapenda kufanya kazi na Makandarasi wazawa na itahakikisha mapendekezo yote yanayotolewa na CRB yanafanyiwa kazi kwa wakati.

“Jipangeni muwe na uwezo wa kusimamia miradi ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa nasi tutawapa kazi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amewataka CRB kufanya tafiti ili kujiridhisha kama utendaji kazi wa ‘force account’ na ule wa wakandarasi wadogo upi unaleta matokeo chanya kwa Serikali.

Waziri Prof. Mbarawa ameahidi kufuatilia utaratibu wa dhamana kwa wakandarasi ili kuweka mazingira nafuu ya dhamana za Benki na Bima ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Eng. Consolatha Ngimbwa, ameiomba Serikali kutoa fursa nyingi za ujenzi kwa makandarasi wanaohusika na ujenzi wapatao 4,500 sawa na asilimia 36 ya makandarasi wote ili kuhuisha Sekta ya Ujenzi ambao imeathririka kutoka na uwepo wa ujenzi unaotumia ‘force account’.

Eng. Ngimbwa amewataka Makandarasi kushirikiana ili kujengana uwezo na kuiomba Serikali kutoa baadhi ya kazi katika miradi mikubwa inayojengwa na makandarasi wa nje ili kuwajengea uwezo na uzoefu.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi hiyo, Rhoben Nkori, amesema zaidi ya makandarasi 12,993 wamesajiliwa na Bodi hiyo ambapo katika mkutano huo pamoja na mambo mengine watalaamu hao watapata fursa ya kujadili, kubadilsha na uzoefu na kupatia ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili makandarasi nchini.