Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

Waziri Chamuriho ambana Mkandarasi barabara ya Kuseni - Suguti


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amemtaka Mkandarasi Kampuni ya Gemen anayejenga barabara ya Kuseni hadi Suguti (Km 5) kwa kiwango cha lami, kuhakikisha  anakamilisha barabara hiyo haraka kama ilivyo kwenye mkataba.

Hayo yamesemwa na Waziri huyo mkoani Mara, wakati akikagua mradi huo ambao unatekelezwa kwa gharama ya kiasi cha shilingi Bilioni 8.2 na kutarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.

Aidha, Waziri Chamuriho, amempa Mkandarasi huyo siku 14 kuhakikisha analipa madai ya mishahara ya wafanyakazi zaidi ya 30 ambao wanadai Kampuni hiyo zaidi ya miezi Nane hali inayopelekea wafanyakazi hao kushindwa kujikimu kimaisha.

“Mkandarasi hakikisha unamaliza mradi huu haraka kama ilivyo kwenye mkataba, kasi mlionayo bado haijaniridhisha, pia hakikisha unawalipa wafanyakazi wako mishahara yao ndani ya siku 14”, amesema Chamuriho.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mara, Mhandisi, Ngaile Mlima, amesema kuwa tayari Mkandarasi huyo ameshalipwa malipo ya awali ya kazi hiyo, hivyo hakuna sababu ya Mkandarasi huyo kutokumaliza mradi kwa wakati.

Ametaja kazi zilizofanyika ni pamoja na kujaza changarawe, ujenzi wa tabaka la chini la barabara, ujenzi wa miundombinu ya maji pamoja na ujenzi wa makalvati saba kati ya nane ambapo yamekamilika.

Ameongeza kuwa kazi zinazotarajiwa kufanyika sasa ni ujenzi wa tabaka la kati na la juu la barabara pamoja na ujenzi wa lami ya juu ya barabara ambapo amesema kuwa kazi zitaanza mara moja kuanzia sasa.

Naye, Issa Sikonya, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni ya kikandarasi ya Gemen amelalamika mbele ya Waziri Chamuriho kuwa Mkandarasi anasuasua kuwalipa stahili zao za mishahara na hivyo kushindwa kupata hata hela ya kula hivyo anaamini mkandarasi atatekeleza agizo hilo kwa haraka.

Waziri Chamuriho yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mara ambapo pamoja na mambo mengine amekagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kuseni hadi Suguti(Km 5) kwa kiwango cha lami, ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.