Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

WAJUMBE ROAD FUND BOARD WARIDHIKA NA UJENZI KITENGULE


Wajumbe wa bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), wametembelea na kukagua ujenzi wa Daraja la Kitengule linalounganisha Wilaya za Misenyi na Karagwe mkoani Kagera.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa daraja hilo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Joseph Haule amesema kuwa mradi wa ujenzi wa daraja hilo umeenda vizuri na umekamilika isipokuwa barabara unganishi ambazo zinatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.

“Lengo la safari yetu ni kuja kujifunza namna ambavyo miundombinu hasa ya barabara inavyoweza kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi hii na hivyo kufahamu kama kuna changamoto zozote wanazipitia katika utekelezaji wa mradi huu” amesema Haule.

Haule ameongeza kuwa Bodi imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo na kuwa wamechukua changamoto zilizopo ili kuzifanyia kazi na hatimae kuhakikisha kuwa daraja hilo pamoja na barabara unganishi zinakamilika ili kuongeza tija katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

 Kwa Upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara(TANROADS), mkoa wa Kagera Mhandisi Yudas Msangi, amesema kuwa ujenzi wa Daraja la Kitengule pamoja na barabara unganishi unagharimu jumla ya Shilingi Bilioni 26 na kwamba katika utekelezaji wa mradi huo Serikali imeonesha nia ya kujenga kipande cha barabara  chenye urefu wa Kilometa 25 zaidi kutoka mradi wa awali unapoishia kwenda hadi Misenyi

Naye Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Mhandisi Lucas Nyaki, amesema daraja hilo lina urefu wa mita 140 na linajengwa pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa KM 18. Katika daraja hilo mita 70 ni daraja la chuma na mita 70 ni daraja la zege, ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 85.8 na kwamba mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba.

Akizungumzia faida za mradi huo, Vicent Mtaki ambae ni Msaidizi wa Mtendaji Mkuu katika kiwanda cha Sukari cha Kagera ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara unganishi, ameongeza kuwa awali walikuwa wakitumia masaa zaidi ya mawili (2) kufikisha muwa kiwandani kutoka mashambani, lakini sasa wanatumia nusu saa tu kufikisha muwa kiwandani, hali inayoongeza ufanisi na uzalishaji zaidi katika kiwanda hicho.

Awali, Mhandisi Rashid Kalimbaga ambae ni Meneja Msaidizi (Ufundi), kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Bodi imechangia katika hatua za mwanzo za ujenzi wa mradi huo kwa kutoa fedha za usanifu na upembuzi yakinifu kama maandalizi ya mradi, lakini pia Bodi inapita kwenye miradi kama hiyo ili kujiridhisha juu ya viwango vya utekelezaji wa mradi kwa kuwa mradi utakapomalizika Bodi itaanza kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya daraja hilo pamoja na barabara zake.

Daraja la Kitengule linaunganisha barabara kuu ya Kyaka- Bugene- Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction- Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.