Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

Waitara ataka wakandarasi wazawa kuchangamkia fursa


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kufanya utafiti wa kwanini Wahandisi Wazawa hawakuomba kazi licha ya Mkandarasi Kampuni ya SINOHYDRO Corporation Limited kutangaza kazi kwa mradi wa upanuzi wa kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani, Iringa.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho Naibu Waziri Waitara amesema kutoshiriki kwenye miradi mikubwa ya ujenzi kunawanyima uzoefu wahandisi wazawa nchini, hali itakayosababisha kushindwa hata kufanya ukarabati baada ya mradi kukamilika.

“Kama nafasi zinatangazwa kwenye miradi na wahandisi wetu hawaombi kazi hizi, ipo haja ya kufanya utafiti kujua sababu ni ni nini, hivyo nawaagiza TANROADS kufanya  utafiti kuhusu suala hili’, amesema Naibu Waziri Waitara.

Aidha, Naibu Waziri Waitara amezitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na TANROADS kukaa pamoja ili kukubaliana namna ya kutekeleza awamu zote mbili za ujenzi kwa mara moja.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera amesisitiza utekelezaji wa awamu zote mbili za ujenzi kwani utapunguza muda wa utekelezaji na kufanya mradi kukamilika kwa muda mfupi.

Naye Msimamizi wa Mradi kutoka TANROADS Mhandisi, Wenceslaus Bavuma, amemuhakikishia Naibu Waziri Waitara kuwa Wakala unasimamia kwa karibu mradi huo na utahakikisha viwango vyote vinazingatiwa ili mradi ukamilike kwa wakati na viwango.

Mradi wa kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani Iringa utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 40 na utahusisha urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, jengo la muda la abiria, jengo la zima moto, jengo la kuongozea ndege, taa za barabarani na kituo cha nishati.