Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

WAHITIMU UBAHARIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA UCHUMI WA BULUU


Serikali imewataka wahitimu wa kozi mbalimbali za sekta ndogo ya bahari nchini kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kushauri namna bora za kutumia fursa zilizopo kwenye uchumi wa buluu unaotokana na sekta  hiyo ili kuinua pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Akizungumza katika mahafali ya 18 ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema uchumi wa bluu unawategemea sana wataalam waliohitimu kozi za bahari hasa ukizingatia kuwa sasa Serikali inawekeza katika ujenzi wa miundombinu na meli katika bandari zetu.

“Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya bandari pamoja na ujenzi wa meli katika maziwa yetu yote hii ni katika kutekeleza azma ya kutumia fursa za uchumi wa buluu, hivyo mliohitimu tambueni kuwa Serikali inawategemea sana", amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na uwekezaji huo kwenye miundombinu ameutaka uongozi wa DMI kuhakikisha inaainisha changamoto ikiwemo za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi ili Serikali iongeze nguvu kwenye eneo hilo kwa maslahi mapana ya kuongeza ujuzi kwa vitendo kwa wanafunzi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya DMI, Kapteni Ernest Bupamba, amesema chuo kimeendelea kuongeza kozi katika maeneo mbalimbali ambapo mpaka mwaka 2022 kimeweza kuongeza kozi za shahada ya uzamili kufikia tano kutoka kozi tatu zilizokuwapo kwa mwaka 2021.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Tumain Gurumo, ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa bajeti kwa mwaka 2022/2023 kwa ajili ya ununuzi wa simulator mbili zitakazosaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo kabla ya kuingia baharini.

Katika mahafali ya 18 ya DMI wanafunzi zaidi ya 900 wamehitimu katika wa kozi mbalimbali zikimemo shahada ya uzamili, shahada, astashahada na cheti katika masuala ya bahari.