Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI TAALUMA MUHIMU INAYOSAHAULIKA KATIKA MIPANGO YA UENDELEZAJI WA MIUNDOMBINU NCHINI


Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi ni moja ya taaluma muhimu katika maendeleo ya nchi. Miji mingi duniani imeendelea kutokana na uwepo wa wataalamu hawa kutokana na ukweli kwamba hutumia utaalamu waliokuwa nao kubuni na kushauri namna bora ya utekelezaji na ujenzi wa majengo mbalimbali.

Tanzania kama ilivyo nchi nyingine, haikubaki nyuma katika kuwekeza kwa wataalamu hawa ambapo kwa ujumla wamekuwa wakitumiwa na watu binafsi, makampuni pamoja na Serikali katika kubuni na kutoa ushauri juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo majengo ya Makazi, Biashara, Viwanda, Shule, Hospitali, Ofisi pamoja na miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Wataalam hawa wenye majukumu tofauti yenye kutegemeana wana kazi kubwa ya kuhakikisha miradi inayotekelezwa inazingatia thamani ya fedha kwa kuhakikisha inatazama gharama hizo kwenye ubunifu wa hali ya juu na kupunguza gharama zinzoweza kuepukika.

Kwa kifupi huwa na jicho la pili katika kuhakikisha kuwa gharama za miradi na ujenzi zinaendana na kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na taswira inayovutia.

Halikadhalika ili kuhakikisha Taaluma hii inalindwa na inafanya kazi kwa viwango vya ubora na uhakika Serikali iliamua kuanzisha Bodi ya Usajili wa wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kwa Sheria Na.16 ya mwaka 1997 na kufanyiwa mapitio mwaka 2010.

Bodi hii imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali ikiwemo kusajili wataalam wa fani hii ambapo kwa sasa wamefikia 1,329 kati ya hao Wataalam Wazawa ni 1,295 na Wageni ni 34 kutoka 188 waliokuwepo mwaka 1998.  Vilevile Bodi hii imesajili Kampuni za Ushauri 418 kati ya hizo Kampuni za Wazawa ni 411 na za Wageni 7. Kwa kipindi cha mwaka 2022/23 Bodi imepanga kusajili Wataalam 125 na Kampuni 25 ambapo hili ni ongezeke la 9%.

Aidha, Bodi inazo Taasisi mbili za Kitaaluma inazozisimamia na kushirikiana nazo ambazo ni Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania (Architectural Association of Tanzania – (AAT)) na Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi Tanzania (Tanzania Institute of Quantity Surveyors – (TIQS)).

Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania kilianzishwa mwaka 1982 na Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi Tanzania ilianzishwa mwaka 1987 na kusajiliwa chini ya Sheria za Vyama vya Ushirika.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa AAT na TIQS ni Kuwaunganisha Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi ili kutoa usaidizi kwenye Bodi, Kuratibu Semina Endelevu (CPD), Kutoa Mafunzo kwa Wahitimu, kurahisisha Mawasiliano kati ya Bodi na Wanachama, Ushirikiano na Vyama vya Kitaaluma vya Kimataifa na kutoa Ushauri unaotegemewa na Waendelezaji katika Sekta ya Ujenzi, Ubora na Usimamizi wa Rasilimali Fedha.

Hadi sasa AAT kina Wanachama wapatao 566 na TIQS ina Wanachama wapatao 1,041. Wanachama hawa ni Washirika, Wahitimu na Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Fundi Sanifu.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Mbunifu Majengo Edwin Nnunduma anasema kuwa Ibara ya 34(5) ya Sheria Na. 4 ya mwaka 2010 inazitaka Kampuniu za Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi kusajili kwenye Bodi na kusimamia ujenzi ili kuhakikisha kuwa masharti yote ya ujenzi yanazingatiwa.

Hivyo, kwa mwaka wa fedha 2021/22 Bodi ilipanga kusajili miradi 1,000 ya majenzi ya majengo ya Makazi, Biashara, Viwanda, Huduma za Jamii kama vile Elimu, Afya, majengo ya Ibada nk. Hadi kufikia mwezi Juni, 2022 Bodi imesajili miradi 1,097 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 4,505 ikiwa sawa na asilimia 9.7% zaidi ya lengo. Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Bodi imepanga kusajili miradi ya Majenzi 1,400 na hadi Robo ya Kwanza ya mwaka huu wa fedha Bodi imekwishasajili miradi 305 yenye thamani ya Shilingi Milioni 503.55.

Aidha, Nnunduma alifafanua kuwa tangu mwaka 2020 Bodi imekuwa na utaratibu wa kufanya Mkutano Mkuu wa Mwaka (Annual Conference) kwa Lengo la kutathmini Utendaji Kazi pamoja na Kuwanoa Wataalam ili kuwawezesha kuendana na mabadiliko ya Teknolojia ya Ujenzi.

Alisisitiza kuwa mwaka jana waliweka lengo la kusajili miradi 1,000 lakini waliweza kusajili miradi 1,097 yenye thamani ya Sh4.5 trilioni.

Kuhusu wahitimu katika fani hiyo, Nnunduma alisema takribani wahitimu 250 wanahitimu masomo yao kila mwaka, lakini ni 150 pekee ndiyo wanajiunga na bodi hiyo na kupata fursa ya kupata mafunzo kwa vitendo kwenye taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Pia alifafanua kuwa katika kuhakikisha kwamba Wataalam waliosajiliwa na Bodi wanaendana na mabadliko ya Sayansi na Teknolojia katika taaluma zao, Bodi inawajibika kudhamini, kuandaa na kutoa nyenzo za mafunzo, semina, warsha, kongamano na mashauriano kuhusiana na Taaluma za Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi na sekta ya Ujenzi kwa ujumla.

Katika Mkutano huo ambapo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, alikuwa Mgeni rasmi, alizungumzia umuhimu wa Bodi ya Usajili Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kuongeza idadi ya wataalam wa fani hiyo waliosajiliwa nchini.

Mhe. Mwakibete alisema kuwa Serikali itaendelea kutoa ufadhili wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa fani hiyo kila mwaka ili kuongeza idadi ya wataalamu hao wenye sifa nchini na hivyo kuwawezesha kufanyakazi ndani na nje ya nchi.

" Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kwa uchumi na maendeleo ya nchi hivyo simamieni kikamilifu sekta ya majenzi ili kuboresha miji na kuleta usalama wa majengo," alifafanya Mwakibete.

Mkutano huo ulioongozwa na mada kuu inayosema "uhifadhi wa majengo kwenye miji ya Afrika kwa sasa" ulihudhuriwa na wataalamu mbalimbali katika sekta ya ujenzi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kuhakikisha ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi unakwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Aidha, Mwakibete aliwahakikishia wataalam hao kuwa Serikali itaendelea kutoa ufadhili huo ili kuongeza idadi ya wataalamu wazawa na kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imeidhinisha kiasi cha Shilingi milioni 550 kwa ajili ya Mpango wa Mafunzo ya Wahitimu kwa Vitendo (EAPP).

 Naibu Waziri Mwakibete alitoa wito kwa Bodi hiyo kuziangalia upya gharama za usajili wa wanachama ili ziwe nafuu na hivyo kuwawezesha wataalam wenye sifa kusajiliwa na kuwawezesha wananchi kutumia huduma za wataalam waliosajiliwa. 

Mwakibete alisema kuanzia sasa wataalamu wote watahusishwa katika miradi ya ujenzi na kwamba Wizara yake imeunda timu maalumu kwa ajili ya kupitia miradi inayoendelea na kutathmini mahitaji yanayotakiwa.

"Kuanzia sasa lazima wataalamu wote washirikishwe kwenye miradi, Serikali itatumia wataalamu katika sekta zote ili kukidhi mahitaji ya makundi yote," alisisitiza Mwakibete.

"Natoa rai kwa waendelezaji kuhakikisha wanatumia wataalamu katika miradi ya 'force account'. Serikali tunaamini kwamba force account inapunguza gharama kwa Serikali, kwa hiyo hata nyinyi hamtakiwi kutupa tofauti kubwa," alisema Mwakibete.

Mwenyekiti wa Bodi ya AQRB, Dkt. Ludigija Bulamile, alisema kuna umuhimu wa kushirikisha wataalamu wote katika utekelezaji wa miradi ili kuondoa changamoto zinazojitokeza baada ya kukamilika kwa miradi husika.

Alisema miradi yote inatakiwa kuwa na wataalamu wote, wakiwamo wahandisi, wakandarasi na wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ili kuzingatia mahitaji ya makundi yote yatakayotumia miundombinu.

Hivyo, ili miji na majiji kupendeza na kuwa na majengo bora na imara nchini ni muhimu kushirikisha wataalamu hawa katika miradi ya ujenzi wa miundombinu nchini ikiwemo majengo ya Makazi, Biashara, Viwanda, barabara,madaraja, ujenzi wa viwanja vya ndege, Huduma za Jamii kama vile Elimu, Afya pamoja na majengo ya Ibada.