Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

TMA YAAGIZWA KUBUNI VYANZO VYA MAPATO


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Ally Possi, ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kubuni vyanzo vya mapato ambavyo ni himiilivu na visivyoumiza washitiri ili kuisaidia taasisi kujiendesha na kuendelea kutoa huduma bora na zenye viwango.

 

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Possi amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Mamlaka hiyo na kusema kuwa ongezeko la mapato litapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya watumishi kuhama kwani mapato yataweka mazingira mazuri kwa watumishi.

 

“Nikupongeze sana Mkuu wa Chuo kwani kazi yako inaonekana sababu utabiri kwa sasa ni wa kuaminika kwa asilimia zaidi ya 80 lakini fikirieni kuja na vyanzo vya mapato visivyoumiza washitiri wenu ili mtumie sehemu ya mapato hayo kama motisha kwa watumishi wenu",  amesisitiza Dkt. Possi.

 

Dkt. Possi amesema kuwa Serikali iko tayari kushughulikia changamoto zote zinazoikabili Mamlaka hiyo ikiwemo changamoto za kuhama kwa watumishi ili kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuwa imara.

 

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya hali ya hewa ili kuongeza uhakika wa taarifa kwa kuwa sekta ya hali ya hewa inazitegemeza sana sekta nyingine hususani za usafirishaji pamoja na kilimo.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa Mamlaka imejipanga kikamilifu kuboresha miundombinu pamoja na kusomesha watumishi ili kuendeleza weledi katika sekta hiyo.

 

Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi yuko katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam ya kutembelea taasisi zilizo chini ya sekta hiyo ili kuona shughuli mbalimbali za kiutendaji na kujadili namna bora ya kupata suluhu ya chagamoto zinazowakabili.