Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

TEMESA WAKUTANA NA WADAU KUJADILI UBORESHAJI UTENDAJI KAZI


Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umekutana na wadau kujadili namna bora ya utoaji wa huduma ili kuleta tija, kupunguza malalamiko ya wateja na kuleta mabadiliko na matokeo chanya kuanzia kwenye menejimenti hadi watumishi.

Kikao hicho kilifanyika Mkoani  Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Bwana Ludovick Nduhiye, alisema lengo la kikao hicho ni kupitia na kukusanya maoni kuhusu andiko la mkakati wa maboresho ya wakala huo.

Alisema karakana zisizo na ufanisi zinaleta  gharama kubwa kwa Serikali katika  uendeshaji wake, hivyo wanapitia upya utendeji wa TEMESA ambao utashirikisha pia sekta binafsi ambao ni wadau muhimu.

“Nimefurahishwa sana kuona Mkurugenzi Mkuu wa Toyota kuwa hapa kwani kampuni hiyo ni mdau mkubwa wa Serikali kwenye aina ya magari yanayotumika serikalini pamoja na matengenezo ya magari,” alisema Bwana Nduhiye.

Aliongeza kuwa Serikali imekutana na wadau wake muhimu ili waweze kutoa mtazamo wao kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo, pamoja na kupokea maoni ambayo yanaweza kutoa majawabu  sahihi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala, alisema ana imani kuwa baada ya kuchambua na kuangalia maeneo mbalimbali ya kufanyia maboresho wakala huo utakuja kivingine na kuendana na kasi ya Serikali katika ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Toyota Tanzania, Bwana Kadiva William, alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa wako tayari kama wadau ambao ni waagizaji wakubwa wa magari yanayotumika serikalini kuisaidia Serikali katika namna bora ya kuvilinda vyombo  hivyo ili viendelee kuwa katika hali nzuri na kuiwezesha serikali kupunguza matumizi katika eneo hilo.

Pia aliahidi kuendelea kutoa matengenezo kwa magari mapya hadi yatakapofikia kilometa 76,000 bila gharama yoyote.