Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

TCAA yaongeza Ukusanyaji wa Mapato


Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzanai (TCAA), kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kupitia Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), ambapo katika mwaka huu wa fedha 2020/21  kimeweza kukusanya takribani Shilingi Bilioni 2 kutoka Milioni 500 zilizokusanywa 2017/2018 na hivyo kuongeza mapato ya Mamlaka kufikia zaidi ya Bilioni 45 kwa mwaka.

 

Ameongeza kuwa makusanyo hayo yametokana na uwepo wa miundombinu bora ya chuo  hicho kuwa ya kisasa ikiwemo mifumo ya kisasa ya mafunzo kwa vitendo (Simulator) za kufundishia kozi mbalimbali chuoni hapo.

 

Akizungumza hayo jijini Dar es Salaam, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea Mamlaka hiyo na chuo hicho ambapo pamoja na mambo mengine ameipongeza TCAA kwa kuweka mikakati thabiti katika uthibiti katika usafiri wa anga na kuitaka mamlaka kuendelea kuwekeza katika wataalam ili kukidhi mahitaji ya udhibiti.

 

 “Nakupongeza sana Mkurugenzi Mkuu kwa kuweka mikakati mizuri ya mwendelezo wa taasisi yako, nimefarijika sana kusikia mna miradi ambayo mnaitekeleza kwa kutumia fedha zenu wenyewe kama mradi ya rada nne, hili ni la kupongeza”, amesisitiza Naibu Waziri Atupele.

 

Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Bw. Hamza Johari, amesema pamoja na ongezeko la mapato ya Mamlaka iko kwenye hatua mbalimbali ya kujenga majengo ya kisasa ambayo yatarahisisha utoaji wa elimu chuoni hapo.

 

“Idadi ya wanafunzi tunaopokea imekuwa ikiongezeka na kama ulivyoona tuna madarasa machache sana, ila mipango iliyopo kwa sasa ni hukakikisha tunajenga majengo kwenye eneo uliliona ili wanafunzi wetu wasome kwenye mazingira rafiki", amesema Bw. Johari.

 

Vilevile Mkurugenzi Mkuu amesema pamoja na kuimarisha chuo hicho ambacho kimekuwa sehemu ya pato kwa Mamlaka, mipango mingine iliyowekwa katika kuboresha utendaji ni kuongeza wataalam kwenye fani mbalimbali ili kwenda sambamba na maboresho yanayofanywa na Serikali kuboresha usafiri wa anga.

 

Naibu Waziri Atupele yuko mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kutembelea, kufahamiana na kuzungumza na viongozi na watumishi waliopo katika taasisi za Sekta ya Uchukuzi na pamoja na kukagua miradi ya kisekta.