Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

SERIKALI YAJIPANGA KUONGEZA UFANISI BANDARI YA TANGA


Serikali imesema mikakati madhubuti iliyojiwekea ikiwemo kupunguza tozo mbalimbali zinazotozwa katika bandari nchini itaongeza ufanisi, ushindani na hatimaye kupunguza gharama kwa wafayabiashara wa ndani na nje ya nchi wanaotumia bandari nchini.

 

Akizungumza katika kikao cha Wadau wa maboresho ya Bandari ya Tanga , jijini humo, Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhandisi Aron Kisaka amesema pia mikakati hiyo itapunguza msongamano wa meli katika bandari ya Dar es Salaam na hivyo kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi kutumia bandari.

 

Mhandisi Kisaka ameongeza kuwa pamoja na punguzo ya tozo katika Bandari ya Tanga kwa mwaka wa fedha 2022/23 Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iko katika hatua mbalimbali za kutwaa eneo la Kingoni Wilayani Arumeru ambalo litatumika kama bandari Kavu ili lengo likiwa kupunguza mzigo kukaa bandarini baada ya kupakuliwa hususani kwa mizigo ya wasafirishaji wa Manyara, Arusha, Kilimanjaro na nchi Jirani.

 

“Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza miradi ya miundombinu kwa kasi na imejipnaga kwenye utekelezaji wa maboresho kwa bandari ya Tanga na bandari nyingine ambapo kukamilika kwa miradi hiyo kutachangia uchumi wa Taifa na uchumi wa mikoa ambapo bandari hizo zipo’ Amesema Mhandisi Kisaka.

 

Mhandisi Kisaka ameongeza kuwa vikao vya wadau vinavyofanyika kikanda vimekuwa na tija kwani vimehusisha wadau wote wa Serikali na Sekta binafsi ili kupata suluhu ya pamoja na kupanga mikakati endelevu.

 

Naye Kaimu Meneja wa bandari ya Tanga Masoud Mrisha amesema kuwa wamejipanga kikamilifu kwani Mamlaka imeongeza vifaa ambavyo vinakwenda pamoja na maboresho ya utendaji wa bandari hiyo.

 

Ameongeza kuwa pamoja na utekelezaji wa maamuzi ya vikao hivyo tayari Uongozi wa bandari ya Tanga umeanza zoezi la kutembelea mteja mmoja mmoja kwa lengo la kuhakikisha linavutia wateja wengi zaidi.

 

Vikao vya maboresho ya utendaji wa bandari nchini hufanyika mara moja ya kila mwezi vikiwa na lengo la kuhakikisha changamoto zote zinazowasilishwa na wadau na watumiaji wa bandari zinatatuliwa kwa wakati na kwa ufanisi.