Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

RAIS SAMIA AFUNGUA BARABARA YA NYAHUA - CHAYA KM 85.4 MKOANI TABORA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara na madaraja ili kuifungua na kuunganisha nchi katika kanda zote na hivyo kuchochea maendeleo.

 

Amesema hayo Wilayani Uyui wakati akifungua barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa kilometa 85.4 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.

 

"Barabara zinajengwa kwa fedha nyingi hivyo zitunzeni ili zidumu kwa muda mrefu na zitumieni kukuza shughuli za kiuchumi", amesema Mhe. Samia.

 

Ameonya tabia za baadhi ya watu kuhujumu miundombinu na kusema Serikali itawachukulia hatua kali wanaoendekeza vitendo hivyo kwani licha ya kuidhoofisha miundombinu hiyo pia wanasababisha ajali.

 

"Acheni kuchimba mchanga kwenye hifadhi za barabara na madaraja kwani kufanya hivyo ni kuhujumu miundombinu na kuisababishia Serikali hasara na kero kwa wananchi", amesisitiza Mhe.  Rais.

 

Ameitaka Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara TANROADS  kuhakikisha barabara na madaraja yanajengwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati.

 

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewataka wakazi wa mikoa ya Tabora, Kigoma  na Katavi kuitumia barabara hiyo kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

 

Amesema Wizara itaendelea kuiimarisha Bodi ya Mfuko wa Barabara ili uhudumie barabara nyingi zaidi.

 

Naye Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya umehusisha madaraja makubwa mawili, makalvati makubwa 32 na madogo 60 na umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 123 toka Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait.

 

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo wa Kuwait, Waleed Al-Bahar, ameipongeza Tanzania kwa ujenzi  wa miundombinu na kuahidi kuendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo.

 

Kukamilika kwa barabara ya Nyahua-Chaya (Km 85.4), kunaifanya barabara yote ya Manyoni-Itigi-Tabora (Km 254), kuwa ya kiwango cha lami na hivyo kupunguza msongamano kwenye barabara ya Nzega-Singida-Manyoni.