Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

RAIS SAMIA AAGIZA VIONGOZI KUTUMIA FURSA ZA UJENZI WA BARABARA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa Mikoa na Wilaya nchini kutumia fursa za ujenzi wa barabara kuibua miradi ya maendeleo na uwekezaji ili kuchochea maendeleo kwa wananchi.

 

Amesema hayo wilayani Sikonge wakati akifungua barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa KM 342.9 kwa kiwango cha lami.

 

"Barabara hii inayounganisha mkoa wa Tabora na Katavi itumieni kuvutia wawekezaji na kuhamasisha kilimo na uzalishaji wa asali ili kukuza uchumi wa wananchi wa mikoa ya Ukanda wa Magharibi", amesema Rais Samia.

 

Rais Samia amezungumzia umuhimu wa watanzania kutunza na kulinda miundombinu ya barabara na madaraja ili idumu kwa muda mrefu na wote watakaohusika na vitendo vya uhujumu miundombinu hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.

 

"Tunzeni miundombinu kwa manufaa yenu wenyewe kumbukeni maendeleo ni safari na kila safari huanza na hatua za awali", amesisitiza Rais Samia.

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imepanga kuunganisha barabara ya Kagwila - Karema ili  kuvutiwa wasafirishaji wa kwenda DRC kutumia njia hiyo hali itakayochochea maendeleo ya mikoa ya Kanda ya Magharibi.

 

Amesisitiza kuwa Serikali  ina mpango wa kujenga barabara za Ipole - Rungwa na Mpanda-Uvinza kwa kiwango cha lami ili kukuza fursa za kilimo, mifugo, utaliii katika hifadhi ya Katavi na biashara kati ya Tanzania na nchi za DRC, Rwanda, Burundi na Zambia na hivyo kukuza Uchumi.

 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini,  Eng.  Rogatus Mativila,  amesema barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa kilometa 342.9 ambayo imesanifiwa kubeba uzito wa magari yenye tani 65 imegharimu  shilingi Bilioni 473.95 ambazo ni mkopo nafuu toka Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB).

 

Barabara ya Tabora – Koga – Mpanda yenye urefu wa kilometa 342.9 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami ni barabara kuu inayounganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Tabora.