Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

PROF. MBARAWA DARAJA LA WAMI KUKAMILIKA JULAI


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayejenga Daraja la Wami na barabara unganishi kampuni ya Power Construction Corporation Limited ya nchini China ili akamilishe ujenzi huo ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

 

Akizungumza mara baada kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 75.7 Prof. Mbarawa amesema kazi zilizobaki zifanyike usiku na mchana ili ujenzi huo  ukamilike haraka na kwa viwango vilivvyokusudiwa.

 

“Daraja hili lenye urefu wa Mita 510 na barabara unganishi zenye urefu wa Kilomita 3.8, vyote vikamilike ifikapo Julai mwaka huu’ amesisitiza Waziri Prof Mbarawa.

 

Waziri Prof. Mbarawa amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa wakati kwa miradi yote inayoendelea  nchini ili kuwawezesha wakandarasi kukosa visiingizio vya kuchelewesha miradi nchini na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zinazoletwa na miradi hiyo.

 

“Tumejipanga kuhakikisha miradi yote ya ujenzi wa barabara, mdaraja na vivuko inayoendelea inakamilika kama ilivyokusudiwa, hivyo wote mliopata bahari ya kusimamia miradi hiyo fanyeni kazi kwa uzalengo ilikupata thamani ya fedha”amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

 

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu kwa namna anavyowezesha miradi ya kimmkakati ya WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi kutekelezwa na kuitaja miradi hiyo kuwa ni Barabara ya Bagamoyo-Pangani Tanga hadi Lamu, Daraja la Kigongo-Busisi, barabara ya mzunguko mkoani Dodoma, Viwanja vya ndege vya Msalato, Mtwara, Musoma, Songea na Iring ambayo ikikamilika itaibadili sura ya Tanzania kiuchumi na kijamii.

 

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage amesema ujenzi wa daraja jipya la Wami lenye upana wa kuwezesha magari mawili kupishana  kwa wakati mmoja utaondoa adha ya daraja la zamani lililojengwa mwaka 1959 ambalo haliendani na mahitaji ya sasa.

 

Mhandisi Mwambage amesema daraja jipya litapunguza ajali na msongamano katika barabara ya Chalinze hadi Segera na hivyo kuongeza tija kwa watumiaji wa barabara hiyo.

 

“Faida nyingine tunayoipata kutokana na mradi huu ni kuwezesha wataalam wetu kupata utaalam wa kujenga madaraja makubwa ya kiwango hiki na zaidi ya wafanyakazi 400 wamepata ajira kulipitia mradi huu” amesema Mhandisi Mwambage.

 

Ujenzi wa daraja la Wami ni mwendelezo wa mikakati ya Serikali ya kufungua barabara kuu ili kuwezesha huduma za usafiri na uchukuzi kuwa za uhakika na zinazoaminika na hivyo kuvutia wawekezaji na kurahisisha huduma za uchukuzi nchini.