Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

PROF. MBARAWA AZINDUA BODI YA USHAURI YA TBA


WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuuwezesha Wakala huo kuwekeza kikamilifu katika viwanja vyake  vilivyopo katika maeneo ya kimkakati   ili kumaliza tatizo la upungufu wa nyumba za viongozi na watumishi wa umma lililopo nchini.

Akizungumza mara baada ya kuzindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema huu ndio wakati wa TBA kujiimarisha kimiundombinu na kiuchumi kwa kutumia fursa ya mahitaji ya nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma na majengo ya kibiashara katika miji mikuu.

"..Hakikisheni mnakuja na mipango ya kutumia rasilimali ya viwanja na majengo mlio nayo kupata faida kwa kujenga majengo mazuri katika maeneo ya miji na kuhakikisha nyumba zenu zaidi ya elfu sita zilizopo zinakuwa katika viwango bora wakati wote na kuvutia wapangaji," amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameipongeza TBA, kwa mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi 3,500 Nzuguni Jijini Dodoma na kuongeza kuwa mradi huo ukikamilika kwa wakati utawaongezea mapato kwa kuwa bado mahitaji ya nyumba za viongozi na watumishi wa umma katika maeneo ya mijini ni makubwa.

"...Tengenezeni mikakati ya ubunifu itakayo wawezesha kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha sekta ya majenzi na makazi ya viongozi na watumishi wa umma inaimarika," amesisitiza Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Arch. Dk. Ombeni Swai amesema Bodi yake itafanya kazi kwa uadilifu na ubunifu ili kuiwezesha TBA kupata faida na kutoa huduma ya kuaminika kwa Watanzania.

Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa miongozo anayoitoa na kusisitiza kuwa TBA itaendelea kusimamia mifumo, nidhamu, udhibiti na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya nyumba na majengo ya Serikali nchini kote kwa kuzingatia mahitaji na faida ili kukuza mtaji ikiwemo ujenzi wa nyumba 3,500 jijini Dodoma.

Wajumbe wapya wa Bodi ya Ushauri ya TBA itakayohudumu kwa miaka mitatu ni pamoja na Arch. Dk. Ombeni Swai (Mwenyekiti), Qs. Optatus Kanyesi (Mjumbe), Bw. Shaban Kabunga (Mjumbe), Qs. Joseph Mkali (Mjumbe), na Bi. Vicky Jengo (Mjumbe).