Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

PROF. MBARAWA AWATAKA WANAKIGOMA KUIBUA FURSA UJENZI KIWANJA CHA NDEGE


WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Kigoma ni muendelezo wa mkakati wa Serikali wa kuufungua kwa anga ukanda wa magharibi mwa Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini ujenzi wa jengo la abiria na mnara wa kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Kigoma Prof. Mbarawa amesema mikakati inaendelea na nia ya Serikali ni kuhakikisha kiwanja cha ndege cha Tabora, Sumbawanga na Shinyanga navyo vinaboreshwa.

“ Serikali inafanya bidii kuendeleza usafiri wa anga, maji, reli na barabara kazi kwenu wananchi ni kutumia fursa hizo kukuza kilimo, biashara, utalii na huduma ili maendeleo ya miundombinu yaendane na maendeleo ya jamii kiuchumi”, amesema Prof. Mbarawa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutakiongezea hadhi kiwanja cha ndege cha Kigoma na kuwezesha ndege nyingi kubwa kutumia kiwanja hicho.

Amesema ujenzi huo pia utahusisha uzio wa kiwanja na barabara za kuingia na kutoka katika kiwanja hicho ambapo mkandatrasi kampuni ya China Railway Engineering Group Company Ltd toka China ameshinda kujenga kiwanja hicho kwa muda wa miezi 18 na gharama ya shilingi bilioni 46.68.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaofanyika mkoani Kigoma na kuahidi kukamilika kwa kiwanja cha ndege hicho kutachochea sana biashara ya matunda na mboga za majani mkoani humo.