Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

PROF. MBARAWA AWAFUNDA WADAU WA UJENZI WA BARABARA NA DARAJA LA PANGANI


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewataka wadau wote wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi wa barabara  ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa Kilomita 120.8  inayojengwa kwa kiwango cha lami na daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 kujenga uelewa wa pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano ili mradi huo uanze mara moja na kukamilika kwa wakati.

 

Akizugumza mara baada ya kuzindua rasmi warsha ya maandalizi ya ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni Prof. Mbarawa amesema wananchi wa mikoa ya Pwani na Tanga watanufaika wakati wa ujenzi na mradi huo utakapokamilika.

 

“Hakikisheni changamoto zote za fidia na uhamishaji wa miundombinu iliyopko katika hifadhi ya barabara inaondolewa mara moja ili kazi inapoanza kusiwe na malalamiko wala athari kwa wananchi “amesema Prof Mbarawa.

 

Waziri Prof. Mbarawa ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa gharama nafuu utakaogharamia mradi huu na kuwataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kusimamia kwa ukamilifu ili mradi ukamilike kulingana na mkataba.

 

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila amesema ujenzi wa barabara  ya Mkange-Tungamaa hadi Pangani ni sehemu ya barabara kuu inayoanzia Malindi-Mombasa-Lungalunga-Horohoro-Tanga-Pangani hadi Bagamoyo yenye urefu wa KM 452 ambayo ni barabara ya Afrika Mashariki na taratibu zote za mradi huu zimekamilika.

 

Naye Muwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye ni Mkurugenzi wa Miudmbonu wa Jumuiya hiyo Dkt. Kamugisha Kazaura amesema  mradi huo ni wa kipaumbele katika Jumuiya kwakuwa utakuza bishara katika kanda na hivyo kukuza uchumi wa kanda kwa jumuiya hiyo na watu wake.

 

Dkt. Kazaura Amesema EAC itashirikiana kikamilifu na Nchi wanachama ili kuhakikisha miradi ya vipaumbele inafanikiwa ili kuchochea uchumi wan chi wanachama.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubak Kunenge amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa maeneo ya mradi unapotekelezwa yatasimamiwa kikamilifu ili kukamilika kwa wakati na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa za mradi huo.

 

Katika hatua nyingine amekagua mradi wa upanuzi wa bandari ya Tanga na kuutaka uongozi wa bandari mkoani humo kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili upanuzi huo ukamilike kwa wakati.

 

Amesema upanuzi wa awali wa mita 150 na kina cha mita 14 unaofanywa na Kampuni ya China Harbour Enginering Company (CHEC) ukamilike ifikapo mwezi mei mwaka huu.

 

“Serikali imejipanga kufanya upanuzi wa mita 450 katika bandari ya Tanga ili kuifanya ya kisasa, hivyo hakikisheni mita 150 zinazojengwa sasa zinakamilika ili Kurusu shehena ya mizigo kuanza kushushwa na kupakiwa katika bandari hii’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

 

Waziri Prof. amesisitiza umuhimu wa TPA kuongeza wanafunzi walio katika mazoezi kwa vitendo kutoka vyuo mbalimbali ili kuwajengea uwezo kufuatia miradi  ya ujenzi inayotekelezwa nchini.

 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Adam Malima amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa kufatilia kwa karibu maendeleo  ya miradi inayotekelezwa chini ya Wizara na kusema kukamilika kwa miradi ya barabara, bandari na madaraja kutahuisha uchumi wa Mkoa wa Tanga na watu wake kwa ujumla..