Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

PROF. MBARAWA ATOA SIKU 14 UJENZI DARAJA LA TAZARA


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ametoa siku 14 kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia TAZARA kukamilisha ujenzi wa daraja lililosombwa na maji  katika sehemu ya Fuga-Kisaki KM 211 mkoani Morogoro.

Akizungumza mara baada ya kukagua eneo hilo Prof. Mbarawa amewataka watendaji hao kushirikiana na watendaji wenzao wa TANROADS na TRC ili eneo hilo likamilike haraka na safari za treni za mizigo na abiria ziendelee.

“Hakikisheni katika muda wa siku 7 hadi 14 sehemu hii inakamilika, ujenzi ufanyike mchana na usiku ili kuirudisha reli katika hali yake ya kawaida na hivyo kuondoa usumbufu kwa wateja wenu”, amesisistiza Prof. Mbarawa.

Reli ya TAZARA sehemu ya Fuga-Kisaki KM 211 mkoani Morogoro ilisombwa na maji Februari 14 mwaka huu na kuathiri huduma za usafiri na uchukuzi wa reli hiyo.

Mkurugenzi mkuu wa TAZARA Eng. Bruno Ching’andu amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa jitihada za kuwawezesha kupata vifaa vya kujenga daraja hilo na kumhakikishia litakamilika na huduma kurejea katika kipindi cha wiki mbili.