Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

PROF. MBARAWA ATOA MIEZI MITATU UKARABATI MV. KAZI


WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi Songoro Marine anayefanya ukarabati mkubwa wa Kivuko cha MV. Kazi kuhakikisha kivuko hicho kinakamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

 

Akizungumza alipokagua ukarabati wa kivuko hicho leo jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema Serikali imeshapata fedha kwa ajili ya ukarabati huo, hivyo ni wajibu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) na Mkandarasi Songoro Marine kuhakikisha taratibu za manunuzi na mikataba ya kazi hiyo inakamilika kwa haraka.

 

"...Hakikisheni ifikapo Ijumaa ya Aprili Mosi taratibu za mikataba ziwe zimekamilika na kasi ya ujenzi na uagizaji vifaa nje ya nchi kwa ajili ya kazi hiyo iongezeke ili kufikia lengo," amesisitiza Prof. Mbarawa.

 

 Prof. Mbarawa amesema idadi ya wakazi wa Kigamboni wanaohitaji huduma ya kivuko imekuwa ikiongezeka siku hadi siku hivyo kuwataka TEMESA kutengeneza ratiba maalum ya ukarabati wa vivuko vyake ili kuondoa usumbufu pindi vinapokwenda matengenezo.

 

"Serikali imetenga fedha katika bajeti ijayo ya ujenzi wa kivuko kipya kikubwa kitakachokuwa na uwezo wa kubeba abiria elfu tatu kwa wakati mmoja hivyo TEMESA jipangeni kuendana na kasi ya Serikali," amesisitiza Prof. Mbarawa.

 

 Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Bi. Fatma Almas Nyangasa amemshukuru Prof. Mbarawa kwa mikakati inayofanywa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuboresha huduma za usafiri kwa wakazi wa Kigamboni, na kumuomba aangalie upya viwango vya gharama zinazotozwa kwa mabasi ya abiria yanayotumia Daraja la Nyerere.

 

"...Kupungua kwa gharama za mabasi ya abiria katika Daraja la Nyerere kutapunguza msongamano wa magari katika kivuko cha Magogoni na hivyo kupunguza msongamano kwa kuwa magari mengi yatapita darajani," amesema Bi. Nyangasa.

 

 Naye Meneja wa Ujenzi wa Vivuko TEMESA, Eng. Lukombe Kingo'mbe amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa TEMESA imejipanga kusimamia vizuri ukarabati wa Kivuko cha MV. Kazi na Kivuko kipya kitakachoanza kujengwa baadaye mwaka huu.

 

Zaidi ya abiria laki moja hadi laki moja na elfu hamsini kwa sasa wanakadiriwa kutumia huduma za vivuko kati ya Kigamboni na Feri kwa siku jijini Dar es Salaam.