Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

NAIBU WAZIRI ENG. KASEKENYA ARIDHISHWA NA MAANDALIZI UJENZI WA BRT III


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya ametembelea Ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka BRT na kueleza kuridhishwa kwake na maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi huo kutokea Katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere hadi Gongolamboto KM 24.3.

Naibu Waziri Kasekenya katika ziara hiyo amemkagua atua ya awali ya Mkandarasi Kampuni ya Sinohydro aliyeanza kukusanya vifaa na mitambo ya kuanza kazi ya ujenzi wa Awamu ya Tatu ya BRT.

Amesema mitambo aliyoiona eneo la mradi inaonesha namna Mkandarasi Sinohydro alivyojipanga kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

"...Mkandarasi huyu ndiye anayejenga pia awamu ya pili ya BRT, kwa maana ya uandaaji wa vifaa kwenye eneo la mradi inaridhisha kabisa na maandalizi haya, "...Kwa maana ya kujiandaa kwa kweli amejipanga, nimeongea pia na Mhandisi Mshauri kwenye mikataba kuna vitu ambavyo Mkandarasi inabidi avilete na tayari amevileta hivyo tuna hakika atafanya kazi nzuri," alisema Naibu Waziri Kasekenya.

Ameagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanafanya uchunguzi ili kujiridhisha na wataalam walioletwa kutekelezwa mradi huo kama ndivyo walioainishwa kwenye makubaliano ya mkataba huo. 

"Wataalam wanatakiwa wa aina fulani na aina fulani wote wawepo pamoja na vifaa kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, fanyeni ufuatiliaji kujiridhisha maana kama hatakuwa na wataalam wa kutosha basi ndipo itakapoanza changamoto katika utekelezaji mradi.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha changamoto zote za foleni na msongamano katika usafiri kwa jiji la Dar es Saalam linamalizika mara baada ya kukamilika kwa miradi hiyo.

"Serikali inataka kuona ndani ya Dar es Salaam wananchi wanafanya shughuli zao kwa uharaka na kwa unafuu Zaidi,” alisema Naibu Waziri.

Akizungumza mara baada ya maelekezo ya Naibu Waziri, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, Eng. Harun Senkuku  amesema wamepokea maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi kama ilivyoelekezwa.

Alisema wapo karibu kufuatilia utekelezaji wa mradi huo hatua kwa hatua na watahakikisha unakamilika kwa wakati. Alisema watahakikisha mradi unatekelezwa kwa viwango na ubora kama ilivyopangwa.

"...Tunamhakikishia Mhe. Naibu Waziri Kasekenya kuwa tumejipanga na tupo pamoja na mkandarasi na tutahakikisha tunakuwa na matokeo bora ya kazi hii." alisema Eng. Senkuku.