Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

MWAKIBETE AAGIZA TPA KULETA WATUMISHI BANDARI YA LINDI


Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amempa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wiki mbili kuhakikisha analeta watumishi wa kudumu katika Bandari ya Lindi ili kurahisisiha usafirishaji wa abiria na mizigo katika Bandari hiyo.

Akizungumza mkoani Lindi mara baada ya kutembelea Bandari hiyo Naibu Waziri Mwakibete pamoja na maelekezo hayo amesisitiza umuhimu wa Bandari kufanya vikao na wadau wote ili kuwa na mkakati wa pamoja wa namna ya kuifanya bandari hiyo kurejea katika ufanisi kama awali.

“Bandari hii naelezwa ilikuwa inahudumia mzigo mkubwa sana miaka ya nyuma lakini kwa sasa inaonekana imepoa sana na hakuna mzigo unaosafirishwa hapa wakati gharama za mzigo kwa kusafirisha kwenye maji ni rahisi kuliko kuupitisha barabarani", amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameeleza kuwa kwa sasa Serikali imeamua kupunguza tozo kwa asilimia 30 kwa mizigo inayosafirishwa kupitia Bandari za Mtwara na Lindi ili kuruhusu mzigo mkubwa kupita bandarini ili kuongeza ufanisi kwa utendaji wa Bandari hizo.

Naye, Mbunge wa Lindi Mjini, Hamida Abdallah, ameiomba Serikali kuiboresha Bandari hiyo kwani hapo awali ilikuwa ni eneo ambalo lilitoa ajira na kukuza pato la mkoa kwa usafirishaji mkubwa wa bidhaa za mbalimbali ikiwemo mbao na saruji.

“Mhe Naibu Waziri Bandari hii ilikuwa inasafirisha mizigo na ilifika mahala mpaka meli za Zanzibar zilikuwa zinakuja hapa kuchukua mizigo lakini kwa sasa tunapokea meli ndogondogo ambazo zinabeba mzigo mdogo na kufanya ufanisi usionekane", amefafanua Mhe. Hamida.

Awali akitoa taarifa ya Bandari, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdilah Salim, amesema miongoni mwa juhudi zinazofanywa na TPA kwa sasa ni kuendelea na kufanya upembuzi yakinifu lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya kibandari, vyombo vya kuhudumia shehena na meli ili kuruhusu bandari kufanya kazi wakati wote.

Bandari ya Lindi kwa mwaka wa fedha  2021/2022 imehudumia shehena ya tani zaidi ya 8,574 ambazo zinajumuisha mizigo mbalimbali ikiwemo mazao ya miti pamoja na bidhaa nyingine.