Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

MBARAWA ARIDHISHWA MAENDELEO DODOMA OUTER RING ROAD


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameelezea kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 112.3.

 

Prof. Mbarawa ameyasema hayo mara baada ya kukagua barabara hiyo ambayo ujenzi wake umegawanywa kwenye sehemu mbili, ambazo ni Nala-Veyula-Mtumba yenye urefu wa kilomita 52.3 na Ihumwa-Matumbulu-Nala yenye urefu wa kilomita 60.

 

“Hakikisheni barabara hizi zinakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa na watumishi wote watakaojiusisha na vitendo vya wizi wa mafuta au vifaa kwa nia ya kuhujumu mradi huu wachukuliwe hatua kali za kisheria,” amesema Prof. Mbarawa.

 

Waziri huyo amesema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha malipo yote ya Wakandarasi wa barabara hiyo yanalipwa kwa wakati hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili ujenzi huo ukamilike mapema iwezekanavyo.

 

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dodoma Eng.  Leonard Chimagu amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara hizo utasimamiwa kikamilifu  na watakaobainika kufanya vitendo vya hujuma watachukuliwa hatua kali.

 

Msimamizi wa mradi huo sehemu ya kwanza kutoka Nala-Veyula-Mtumba (Km 52.3), Eng. John Koroso amesema wamejipanga kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyolingana na thamani ya fedha.

 

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutunukiwa tuzo kutokana na mchango wake katika ujenzi na usimamizi wa miundombinu  nchini.

 

Amewataka watumishi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Taasisi zake kutumia tuzo hiyo kama chachu ya kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili kuleta tija na ufanisi katika sekta ya miunndombinu nchini.

 

 

Barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma ( Dodoma City Outer Dual Carriageway Ring Road), inatarajiwa kukamilika Machi 2025, ambapo pamoja na mambo mengine  itapunguza msongamano  katika jiji la Dodoma na kuchochea  shughuli za kiuchumi.