Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

KIWANJA CHA NDEGE CHA MOSHI KUKAMILIKA NOVEMBA MWAKANI


Imeelezwa kuwa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Moshi mkoani Kilimanjaro unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2023 ili kuruhusu ndege zenye uwezo wakubeba abiria 40 za  binafsi na za biashara kuweza kuruka na kutua kiwanjani hapo.

Akizungumza mkoani humo mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amefafanua kuwa baada ya filamu ya Royal Tour iliyofanywa na Rais wa Jamhuri wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu kumekuwa na ongezeko la watalii nchini hivyo dhamira ya Serikali ni kuendeleza miundombinu ya viwanja vya ndege nchini ili kutokwamisha matokeo ya filamu hiyo.

“Uzinduzi wa filamu ya royal tour umekuwa na matokeo chanya ambao tunashuhudia idadi ya watalii inavyoongezeka kila siku, kwa ongezeko hilo ndio maana mnaona tunajitahidi kuboresha viwanja vya ndege ili kuruhusu watalii kuchagua popote wanapotaka kuruka na kutua," amefafanua Naibu Waziri Mwakibete.

Aidha, Naibu Waziri huyo amezitaka Taasisi za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi mzawa anayeboresha kiwanja hicho ili akamilishe kazi hiyo kwa wakati na kwa viwango.

Mwakibete ameutaka uongozi wa TAA, TANROADS na Mkoa kukaa na kumaliza changamoto zilizopo ikiwemo uvamizi wa eneo la kiwanja ili kutomchelewesha mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Kilimanjaro, Eng. Motta Kyando, ameeleza kuwa upanuzi wa kiwanja hicho unagharimiwa na fedha za ndani  kiasi cha zaidi shilingi bilioni 12 na tayari Mkandarasi kampuni ya kizalendo ya Rocktronic Limited ameanza kazi za awali za upanuzi ambapo mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 12.

Eng. Motta ameongeza kuwa upanuzi huo utahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya maegesho ya ndege, barabara za usalama kiwanjani hapo kwa kiwango cha lami pamoja na uzio.

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja hicho, Yusufu Sood, amesema kwa sasa kiwanja hicho kinahudumia ndege ndogo ambazo si za ratiba zinazoweza kubeba abiria mpaka saba na helikopta za watu binafsi hivyo kukamilika kwa maboresho hayo kutaongeza miruko ya ndege na idadi ya abiria.

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku mbili ambapo anakagua miradi ya miundombinu ambayo inatekelezwa na Wizara kupitia Taasisi za Sekta ya Uchukuzi.