Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

KASEKENYA AWATAKA MAKANDARASI KUWAJIBIKA KIFIKRA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amewataka makandarasi, waajiri na wasimamizi wa mradi kuwa na ushirikiano mzuri ili kuwezesha miradi ya ujenzi inayofanyika nchini kuwa ya viwango bora.

Akifunga mkutano wa siku mbili wa mwaka wa mashauriano wa makandarasi jijini Dodoma, Eng. Kasekenya amewataka makandarasi kuwa waadilifu na wanaofanya kazi kwa weledi ili miradi inayojengwa nchini iwiane na thamani ya fedha.

“Kumbukeni kuwa kila haki ina wajibu hivyo mkitekeleza wajibu wenu kikamilifu mtawawezesha waajiri kuwapa haki zenu kwa wakati”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Amezungumzia umuhimu wa makandarasi kushirikiana na wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), ili kupata taarifa sahihi kabla ya utekelezaji wa miradi yao

Kasekenya amewaahidi makandarasi kuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itafanyia kazi maazimio yao yote ili kuhakikisha changamoto za makandarasi na wadau wengine wa ujenzi zinapatiwa ufumbuzi.

“Wajibikeni kifikra ili miradi yenu mnayoitekeleza iwe ya viwango bora na hivyo kuwatendea haki watanzania na kukuza sekta ya makandarasi hapa nchini”, amesema Naibu Waziri Kasekeya.

Naye, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Rhoben Nkori, amezungumzia umuhimu wa waajiri kuheshimu mikataba ya kazi ili kuleta haki, kuepuka vitendo vya kudhalilisha makandarasi wawapo kazini na kutoa fursa kwa makandarasi wazawa katika miradi ili kuwajengea uwezo.

Zaidi ya washiriki 860 wakiwemo makandarasi, wataalam washauri na wadau wa Mamlaka ya Rufaa za Zabuni wameshiriki mkutano huo uliolenga kutathimini umuhimu na mchango wa makandarasi katika uchumi wa Tanzania.