Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAAGIZA DARAJA LA WAMI LILINDWE


Kamati ya Bunge ya Kudumu ya miundombinu imetoa wito kwa wananchi kulitunza Daraja jipya la Wami (m 513.5) na barabara zake unganishi (km 3.8), ili liweze kudumu kwa muda mrefu.

Hayo yamesemwa mkoani Pwani na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, mara baada ya wajumbe wa kamati hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo na barabara zake ambapo wameridhishwa na kazi zilizofanyika mpaka sasa  na kusema kuwa kuwa uwepo wa daraja hilo utakidhi ongezeko la magari yanayopita katika daraja hilo kulinganisha na daraja la zamani.

“ … Kumekuwa na tabia ya kuharibu sana miundombinu ambayo imewekezwa na Serikali pindi inapokamilika wakati miradi hii yote ni mali ya wananchi hivyo muilinde, muitunze kwa kuwa ina manufaa makubwa sana kwa wananchi na Taifa”, amesisitiza Mhe. Kakoso.

Aidha, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya miundombinu imeipongeza Serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 75 katika utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo ambalo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 97 na tayari wananchi wameanza kunufaika na miundombinu hiyo.

 “Kamati inamshukuru Mhe. Rais kwa jitihada kubwa za kuleta maendeleo kwa wananchi ambapo ametoa fedha kwa ujenzi wa daraja jipya la wami ambalo kwa kiwango kikubwa sana litawasaidia wananchi na kuepusha ajali zilizokuwa zikitokea mara kwa mara huko nyuma”, amesema Mwenyekiti huyo.

Kamati hiyo imeshauri Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Pwani kutunza na kuweka na mazingira wezeshi na salama katika daraja hilo kwa kupanda nyasi na miti ili kulifanya daraja hilo liwe endelevu na kutunza uoto wa asili.

Pia imeagiza Wizara ya Ujenzi kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa Daraja la zamani la Wami ili kuongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi na kurahisisha shughuli zao kipindi chote na majira yote.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ameishukuru Kamati kwa kukagua na kujiridhisha na mradi huo na kuiahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo.

Eng. Kasekenya ameeleza kukamilika kwa Daraja jipya la Wami kutasaidia kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwani utapunguza muda wa safari pamoja na ajali zilizokuwa zikitokea mara kwa mara katika daraja la zamani.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani, Eng. Baraka Mwambage, ameieleza Kamati kuwa mradi wa daraja hilo umeajiri jumla ya wafanyakazi 420 ambapo kati ya hao 395 ni wazawa na 25 ni wataalam kutoka nje ya Tanzania.

Eng. Baraka amefafanua kuwa usimamizi na ujenzi wa daraja hilo umewasaidia watalaam wazawa kuongeza ujuzi kutokana na teknolojia mpya iliyotumia katika daraja hilo na kulisaidia Taifa katika ujenzi wa miundombinu kama hiyo hapo mbeleni.

Ujenzi wa Daraja jipya la Wami umetekelezwa kwa fedha za ndani na umesanifiwa kudumu ndani ya kipindi cha miaka 120 ijayo.