Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

KAMATI YA  BUNGE YAAGIZA UJENZI WA DARAJA LA JP MAGUFULI KUKAMILIKA KWA WAKATI


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza serikali kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la JP Magufuli eneo la Kigogo-Busisi Mkoani Mwanza ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Pamoja na kuwasimamia kikamilifu wakandarasi hao, imemtaka Mkandarasi kujitathmini na kuongeza fedha kwa ajili ya huduma za kijamii katika eneo unapotekelezwa mradi huo ili huduma hizo ziweze kuwanufaisha wananchi na kubaki kama alama ya mradi huo mkubwa.

Hayo yamezungumzwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Seleman Kakoso wakati kamati hiyo ilipotembelea na kujionea mradi wa ujenzi wa daraja hilo ambao kwa sasa umefikia asilimia 42.

Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imefika kukagua eneo linapojengwa daraja la JP Magufuli lenye urefu wa kilomita 3.2 ambalo litaunganisha barabara ya Usagara-Sengerema hadi Geita kupitia Ziwa Victoria, na hadi kukamilika kwake litagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 716.

Kasoso amepongeza jitihada ambazo zinaendelea kufanywa na Serikali katika mradi huo ambao Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuutekeleza, pamoja na Wizara kwa usimamizi mzuri ambao umeufanya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuweza kuwasimamia vizuri Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo.

Ameongeza kuwa mambo ya muhimu kuzingatiwa katika mradi huo ni pamoja na kuhakikisha Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo ambao ni China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway Group 15 Bureau Group, wanaukamilisha mradi huo kwa wakati kulingana na matakwa ya mkataba.

 "Simamieni mradi huu kwa karibu zaidi ili Serikali isiingie gharama ya mara kwa mara kwani Wakandarasi wengi wanachelewa pale wanapoona kwamba wanahitaji kuongeza mkataba hasa kwenye fedha zile wanazokuwa wanadai, jambo ambalo kwa sasa Serikali imeanza kutoka kule, nimeona kila mradi tunaouangalia Serikali imeshapeleka fedha, kwa hiyo tunawaomba msimamie kwa karibu ili mradi huu unapokamilika Serikali isibaki na deni," amesema Kasoso.

Sanjari na hayo Kamati hiyo pia imeagiza maslahi ya wafanyakazi wanaoshiriki utekelezaji mradi wa ujenzi wa daraja hilo yasimamiwe kikamilifu ikiwa ni pamoja kuzingatia suala la usalama mahala pa kazi ili kulinda usalama kwa wafanyakazi hao.

Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa kiungo muhimu kati ya mkoa wa Mwanza na mikoa mingine ya Kanda ya ziwa lakini pia nchi za jirani za Rwanda, Burundi na Uganda, na kwamba litakuwa kichocheo kikubwa cha kupunguza umaskini na kuharakisha ukuaji wa uchumi katika eneo la kanda ya ziwa na nchi za maziwa makuu.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo kwa kamati hiyo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 41.59 ambapo mkandarasi ameshatumia siku 753 kati ya siku 1,461 na   ameshalipwa jumla ya Shilingi Bilioni 194 ikiwa ni pamoja na malipo ya awali ya Shilingi Bilioni 87 kwa hati za malipo ambapo mradi huo  ni moja ya miradi ya kimkakati ya Serikali ya kurahisisha usafiri na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imekagua pia vivuko cha MV Sengerema na MV Misungwi vinavyofanya safari zake kati ya Kigongo-Busisi pamoja na ujenzi wa daraja la JP Magufuli mkoani Mwanza.