Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Habari

ERB KUANZA KUJENGA KITUO KIKUBWA CHA UMAHIRI KWA AJILI YA UBUNIFU


Bodi ya usajili wa Wahandisi Nchini (ERB) inatarajia kujenga kituo Kikubwa Cha Umahiri eneo la kizota, Jijini Dodoma ambapo ni Moja ya Vipaumbele vyake ili vijana waweze kufanya shughuli zao kwa kuonyesha ubunifu wao.

Hayo yameelezwa Novemba 10,2022 jijini Dodoma na Msajili wa Bodi hiyo,Mhandisi Bernard Kavishe ,wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya  Bodi hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka 2022/2023

Mhandisi Kavishe amesema kutokana na kuwepo kwa Vijana wengi wenye mawazo ya kibunifu ila wanakosa namna ya kuendeleza mpaka kufika sokoni ,hivyo kituo hicho kitakuwa eneo sahihi la kuendeleza mawazo hayo.

“Kuna vijana wengi wenye mawazo mazuri kabisa ila namna ya kuendeleza inawawia vigumu sana ila tumeona sisi kama bodi suluhisho lake ni kujenga kituo cha umahiri ambapo itatumika kuendeleza vijana na Itakuwa na maabara pia,” Amesema Mhandisi Kavishe

Aidha Mhandisi Kavishe, amesema kuwa rushwa bado ni kikwazo kikubwa katika sekta hiyo nchini hali inayosababisha watu wasio na uwezo kupatiwa kazi katika maeneo mbalimbali.

“Rushwa bado ni kansa ya taifa katika maeneo mbalimbali kweli bado wapo watu ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa lakini sisi tunapo wabaini tunawafikisha katika vyombo vyenye mamlaka na suala hilo kama vile TAKUKURU na wengine”amesema Mhandisi Kavishe.
Vilevile, Mhandisi Kavishe amesema kikwazo kingine wanachokabiliana nacho ni vishoka walipo katika sekta hiyo hivi sasa.

“Vishoka ni ‘crime’ kama ambavyo ilivyo katika tasnia nyingine mtu kujifanya Daktari wakati siyo taaluma yake anastahili kushitakiwa na kufungwa kama mharifu mwingine”amesema

Mhandisi Kavishe amesema kuwa ,kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya Wahandisi 33,773, kati yao 26,000 wapo katika soko la ajiri huku wenye leseni za Uhandisi wakiwa ni 10,000 na wengi wao wanashiriki kwa namna moja au nyingine katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa inayoendelea.

Mhandisi Kavishe amesema kuwa Bodi hiyo imeshasajili Makampuni 398 inayojishuhulisha na masuala ya uhandisi huku makapuni 275 kati ya hayo ni ya ndani ya nchi wakati makampuni 123 yakiwa ni kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa, ameipongeza bodi hiyo kwa namna ambavyo imendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia wahandisi wakati huu ambao taifa likiwa linatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

“Nafasi ya ERB ni kubwa katika maendeleo ya Taifa letu kwani kila penye Mradi unaoendelea ERB wapo na wanathibiti ubora wa kazi na wa Mhandisi anayejenga ule mradi hivyo niwaambieni tu hii ni bodi kongwe na haya majengo mnayoyaona yote kuna Mkono wa ERB”, amesema Msigwa

Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), Imeanzishwa Mwaka 1968, ikiwa na majukumu ya Kusajili Wahandisi,kuendeleza wahandisi na kutoa hithibati kwa waandisi , hayo majukumu yote ERB inayatekeleza kwa ajili ya usalama wa nchi na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele.