Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

DARAJA LA JP MAGUFULI KUPUNGUZA UMBALI WA KM 210.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo - Busisi) utakapokamilika utaokoa muda wa safari wa kutoka Mwanza kwenda Geita umbali wa kilometa 90 tofauti na sasa ambapo wanatumia umbali wa km 210  kupitia Kahama.

Amesema hayo mkoani Mwanza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo ambalo limefikia asilimia 72 ya utekelezaji wake na kutoa fursa za ajira 1,001.

Ameeleza kuwa Daraja hilo likikamilika linatarajiwa kugharimu Tsh. Bilioni 716, ambapo itakuwa ni kama lango la kuingilia Mwanza kutokea mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.

Amesisitiza kuwa ujenzi daraja hilo umezingatia viwango vya juu, linaweza kuwa imara kwa zaidi ya miaka 100.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima ametoa wito kwa wananchi waliopata fursa ya ajira katika mradi huo kutouhujumu kwa kuiba vifaa mbalimbali na kuiongezea Serikali gharama za ujenzi kwani hawamuibii mkandarasi bali wanawaibia watanzania wenzao.

"Tukimkuta mtu ambaye ana vifaa vinavyotokana na mradi huu tutafunga duka na hatafanya tena biashara Mwanza na tutamfungulia kesi ya uhujumu uchumi kisha atatueleza anaoshirikiana nao", amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Ameeleza umuhimu wa Daraja hilo kuwarahisishia watalii wanaopitia Mwanza  kutumia muda mchache kuvuka  na kufanya utalii, hivyo  daraja hili litarahisisha  mawasiliano na kukuza sekta ya  utalii.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya Daraja hilo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila, amesema daraja hilo lina umuhimu kwa wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa jumla, mfano kufika Mwanza kwenda Geita au Sengerema ilikuwa ni lazima uzunguke hadi Kahama, hivyo Daraja la Busisi litaondoa  mzunguko huo.

"Daraja hili litaunganisha watu wa Mwanza, Geita, Kagera na Nchi jirani ya Uganda, kwa huo ukaribu utatumia muda mfupi kwenda nchi nyingine zinazotuzunguka kama Rwanda"amesema Eng. Mativila.

Ameeleza kuwa daraja hilo lilianza kujengwa Mwaka 2020 baada ya mkataba kusainiwa Mwaka 2019 na makubaliano ya mkataba ni kukamilika Februari 25, 2024 kulingana na makubaliano yaliyopo na mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanafikia lengo hilo.