Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Habari

AWAMU YA PILI YA UJENZI WA BARABARA YA ARUSHA – HOLILI KUANZA


Serikali imesema katika kutimiza azma ya kukuza Sekta ya Utalii katika Ukanda wa Kaskazini mwa nchi yetu na nchi jirani ya Kenya, iko mbioni kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa awamu ya pili ya barabara ya Kimataifa ya Arusha – Holili (km 117), Sehemu ya Tengeru – USA River (km 10.1), Sehemu ya Mji wa Moshi (km 8.4) na Ujenzi wa Daraja Jipya la Mto Kikafu lenye urefu wa Mita 560 pamoja na Barabara zake unganishi (km 4).

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati wa ufunguzi wa barabara hiyo kwa awamu ya kwanza sehemu ya Sakina – Tengeru  (km 14.1) kwa njia mbili na Barabara ya Mchepuo ya Jiji la Arusha (km 42.4), uliofunguliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tunatarajia kazi za ujenzi wa barabara hii kwa awamu ya pili kuanza mapema baada ya kukamilika kwa mapitio ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina”, amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema kuwa mkataba wa barabara hiyo ulisainiwa rasmi tarehe 4, Februari 2022 kwa gharama ya Yeni ¥ 24,310,000,000 sawa na Shilingi 413,858,302,000 za kitanzania na utafadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (Japan International Coorperation Agency - JICA), kwa mashart ya mkopo nafuu.

 Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa nyingi za kiuchumi na kijamii ikiwemo kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa, kukuza na kuchochea Utalii wa ndani na nje katika Mbuga zetu hususani Mbuga ya Maajabu Saba ya Dunia – Serengeti National Park na Mbuga nyinginezo za Mlima Kilimanjaro, Mkomazi, Arusha, Ngorongoro, Tarangire na Manyara, pia kupanda Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika.

Aidha uwepo wa barabara hiyo utakuza na kuchochea uzalishaji katika sekta za Kilimo, Viwanda na Ufugaji, kuimarisha ushirikiano na kuchochea Maendeleo ya Biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Hussein Mativila, ameeleza kuwa barabara hiyo inakidhi kiwango cha kujengwa kwa njia mbili kila upande ili kuleta tija zaidi katika shughuli za Kiuchumi na Kijamii. 

Kuhusu Awamu ya Kwanza iliyokwishakamilika kujengwa na kufunguliwa rasmi, Mhandisi Mativila amesema kuwa mradi mzima umegharimu kiasi cha shilingi 197,451,499,951.54 na kufadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank - AfDB) kupitia Mfuko wa Fedha za Maendeleo ya Afrika (Africa Development Fund – ADF).

 Mativila ameongeza kuwa lengo la mradi ni kupunguza msongamano wa magari na muda wa usafiri hasa kwenye Jiji la Arusha kutokana na magari mengi yanayoingia na kutoka katikati ya Jiji. 

 Pia amezitaja kampuni za kikandarasi zilizotekeleza mradi huo ambapo mkandarasi alikuwa ni Hanil kutoka Korea ya Kusini na Jiangsu kutoka China Kampuni iliyosimamia kazi za Ujenzi ni M/s Cheil Engineering Company Ltd kutoka Korea ya Kusini na DOCH Ltd ya Tanzania

Barabara ya Arusha – Holili ni Sehemu ya Barabara Kuu ya Ushoroba wa Kaskazini(Great North Road) ambao pia hujulikana kama Ushoroba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Na. 5 (EAC Corridor no. 5) ambayo inatoka Afrika Kusini (Cape Town) hadi Misri (Cairo) kupitia Zambia na kuingia kwenye Mji wa Tunduma uliopo Mpakani mwa Tanzania na Zambia kwenda Nairobi Kenya, Ethiopia hadi Cairo, Misri.